​BILIONI 100 KILA MWEZI KULIPA MADENI, WAZIRI BALOZI OMAR AWALAINISHA WATUMISHI, WAKANDARASI NA WAZABUNI

Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), akiwasilisha bungeni jijini Dodoma, Mapitio ya Utekelezaji wa Mpango na Bajeti kwa mwaka wa fedha 2025/2026 na Mapendekezo ya Mpango na Bajeti ya Wizara ya Fedha kwa mwaka 2026/2027, ambapo ameliomba Bunge kuidhinisha jumla ya shilingi trilioni 21.3 kwa ajili ya utekelezaji wa majukumu ya Wizara pamoja na taasisi zake kwa Mwaka wa Fedha 2026/27.

Dodoma 2 Juni, 2026: Serikali kupitia Wizara ya Fedha imeliomba Bunge kuidhinisha jumla ya shilingi trilioni 21.3 kwa ajili ya utekelezaji wa majukumu ya Wizara hiyo pamoja na taasisi zake kwa Mwaka wa Fedha 2026/27.

Akiwasilisha Mapendekezo ya Mpango na Bajeti bungeni, Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), alisema fedha hizo zitatumika kugharamia matumizi ya kawaida na maendeleo katika mafungu manane ya Wizara, ambapo kati ya fedha hizo, shilingi trilioni 19.4 zitatumika kwa matumizi ya kawaida huku shilingi trilioni 1.8 zikielekezwa kwenye miradi ya maendeleo.

Alisema kuwa katika Bajeti hiyo, Serikali imepanga kuendelea kusimamia uchumi kwa weledi ili kuhakikisha ukuaji wa uchumi unafikia asilimia 6.3 mwaka 2026 huku mfumuko wa bei ukidhibitiwa kubaki katika katika wigo wa wastani wa asilimia 3 hadi 5.

“Serikali pia inalenga kuimarisha nidhamu ya matumizi ya fedha za umma pamoja na kuongeza ufanisi wa ukusanyaji wa mapato ya ndani” alisema Mhe. Balozi Omar.

Aidha, alibainisha kuwa Wizara imepanga kutenga shilingi bilioni 100 kila mwezi kwa ajili ya kulipa madeni ya watumishi, wakandarasi, wazabuni na watoa huduma ili kupunguza changamoto za malimbikizo ya madeni serikalini.

Kwa upande wa mapato, alisema kuwa Wizara ya Fedha imekadiriwa kukusanya jumla ya shilingi trilioni 55.2, ambapo Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) inatarajiwa kukusanya zaidi ya shilingi trilioni 39.

Katika hatua nyingine, aliliomba Bunge kuiidhinishiwa Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi shilingi bilioni 132.2 kwa ajili ya kuimarisha shughuli za ukaguzi wa matumizi ya fedha za umma pamoja na kuendelea na ujenzi wa ofisi zake katika baadhi ya mikoa nchini.

Comments

Popular posts from this blog

RC CHALAMILA ATAKA MWAROBAINI WA FOLENI DAR UPATIKANE

TANZANIA INAPOTEZA MITI 370,000 KILA MWAKA:NAIBU WAZIRI KWAGILWA NA NMB WAJA NA MKAKATI MPYA WA DIRA 2050