MSIMU WA KIPUPWE 2026: TMA YATAJA MWEZI UTAKAOKUWA NA BARIDI KALI ZAIDI TANZANIA NA HALI YA UPEPO

Dar es Salaam,Tarehe 25/05/2026:

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa rasmi mwelekeo wa hali ya hewa katika kipindi cha mwezi Juni hadi Agosti 2026 (Kipupwe). Akizungumza na waandishi wa habari Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi (IPCC), Dkt. Ladislaus Chang’a aliwataka wananchi kufuatilia na kuutumia ipasavyo utabiri wa msimu wa Kipupwe 2026, hasa ikizingatiwa kuwa katika kipindi hicho baadhi ya maeneo yanatarajia kupata vipindi vichache vya upepo mkali mwezi Juni na Julai 2026.

“Msimu wa Kipupwe 2026 unatarajiwa kutawaliwa na upepo uliopungua nguvu kidogo kama ilivyo kawaida, utakaovuma kutoka Kusini Mashariki kwa maeneo mengi ya nchi, na vipindi vichache vya upepo mkali utakaovuma kutoka kusini hususan katika kipindi cha miezi ya Juni na Julai 2026 hususani katika maeneo ya ukanda wa pwani ya Bahari ya Hindi na maeneo ya nchi kavu”. Alisema Dkt. Chang’a

Akizungumzia hali ya baridi Dkt. Chang’a alisema vipindi vya baridi zaidi vikitarajiwa kujitokeza katika mwezi Julai 2026, aidha, baridi ya wastani hadi joto kiasi inatarajiwa katika baadhi ya maeneo ya nchi.

“Hali ya baridi ya wastani hadi joto kiasi inatarajiwa katika maeneo ya Kanda ya Ziwa Victoria, Kanda ya magharibi, Kanda ya kusini, Nyanda za juu kusini- magharibi pamoja na Mkoa wa Singida. Hata hivyo, hali ya joto kiasi hadi baridi ya wastani ikitarajiwa katika maeneo ya Ukanda wa pwani ya kaskazini na maeneo ya nchi kavu, Nyanda za juu kaskazini mashariki, Ukanda wa pwani ya kusini pamoja na mkoa wa Dodoma huku vipindi vya baridi zaidi vikitarajiwa kujitokeza katika mwezi Julai 2026.” Alisema Dkt. Chang’a.

Akielezea kuhusu mwenendo wa mvua Dkt. Chang’a alisema vipindi vya mvua za nje ya msimu vinatarajiwa katika maeneo ya ukanda wa Ziwa Victoria hususan Mkoa wa Mara, ukanda wa mwambao wa pwani na maeneo ya nchi kavu pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba, na sehemu zenye miinuko za nyanda za juu kaskazini mashariki.

Comments

Popular posts from this blog

RESIDENTS OF IYAGABUYAGA-BUSEGA URGED TO RESPECT WILDLIFE CONSERVATION LAWS

TANZANIA YAKAMILISHA MFUMO WA KUREJESHA HALI BAADA YA MAAFA

RC CHALAMILA MASHINDANO YA AFCON YATUMIKE KIBIASHARA