DKT. MWIGULU NCHEMBA, BWAWA LA NYERERE NA SGR ZAMALIZIKA, SASA NGUVU ZAHAMISHIWA KWENYE BARABARA ZA MIKOA

 

WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba amesema Serikali itaendelea kuwekeza katika miradi ya barabara nchini kwa kuwa ndiyo msingi wa kufungua uchumi, kurahisisha usafirishaji wa mazao na kuchochea maendeleo ya wananchi vijijini na mijini.

“Hizi kilomita 17 zilizobaki kuelekea Dabaga ni eneo muhimu sana la uzalishaji, hivyo Serikali itaendelea kuweka mkazo kuhakikisha eneo hilo linafunguliwa kwa kiwango cha lami,” amesema Dkt. Mwigulu.

Dkt. Mwigulu amesema hayo leo Jumapili, Mei 24, 2026 alipokagua mradi wa ujenzi wa Barabara ya Iringa (Ipogolo) – Kilolo yenye urefu wa kilomita 33.61 kwa kiwango cha lami chini ya Programu ya RISE (Barabara kwa Maendeleo na Fursa za Kiuchumi na Kijamii) katika Wilaya ya Kilolo mkoani Iringa.

Amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kutekeleza miradi ya kimkakati ya miundombinu kwa lengo la kuimarisha shughuli za kiuchumi na kuboresha huduma za usafiri kwa wananchi.

Aidha, Waziri Mkuu amesema Serikali imekubaliana kuhakikisha miradi yote iliyoanza inakamilishwa kwanza sambamba na kuendelea kutoa fedha za utekelezaji kwa miradi iliyosainiwa mikataba lakini haikupata malipo ya awali.

“Tunahakikisha kwanza tunakamilisha miradi ambayo ilikuwa imeanza, iliyosainiwa lakini haikupata malipo ya awali na ile ambayo wakandarasi walishapatikana ili wananchi waanze kunufaika na miradi hiyo,” amesema.

Kadhalika, amesema Serikali imeongeza kasi ya utekelezaji wa miradi mingine baada ya kukamilisha baadhi ya miradi mikubwa ya kimkakati ikiwemo Bwawa la Julius Nyerere, reli ya kisasa ya SGR pamoja na Daraja la Kigongo – Busisi.

“Tuliamua kwanza tumalize miradi mikubwa iliyokuwa imefikia hatua nzuri ili ianze kusaidia uchumi wa nchi. Sasa tunaongeza nguvu kwenye miradi mingine iliyokuwa imepunguza kasi ya utekelezaji wake,” amesema.

Amesema mradi huo wa barabara una umuhimu mkubwa kwa wananchi wa Kilolo kutokana na eneo hilo kuwa miongoni mwa maeneo yenye uzalishaji mkubwa wa mazao ya kilimo mkoani Iringa.

Comments

Popular posts from this blog

RESIDENTS OF IYAGABUYAGA-BUSEGA URGED TO RESPECT WILDLIFE CONSERVATION LAWS

TANZANIA YAKAMILISHA MFUMO WA KUREJESHA HALI BAADA YA MAAFA

RC CHALAMILA MASHINDANO YA AFCON YATUMIKE KIBIASHARA