UNICEF KUBORESHA SHULE MTANDAO NCHINI ILI KUWAWEZESHA WANAFUNZI KUJISOMEA WENYEWE
Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia Watoto Ulimwenguni (UNICEF), Bi. Elke Wisch amekutana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM-TAMISEMI) Mhe. Prof. Riziki Shemdoe na kuahidi kuwa UNICEF itaanzisha na kuboresha shule mtandano (online public schools) ambazo zitawawezesha wanafunzi wa kitanzania kujisomea wenyewe.
Mwakilishi huyo Mkazi wa UNICEF Bi. Elke Wisch ametoa ahadi hiyo Mei 13, 2026 alipomtembelea Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu - TAMISEMI Mhe. Prof. Riziki Shemdoe katika ofisi yake iliyopo Magogoni jijini Dar es Salaam.
Bi. Wisch amemueleza Prof Shemdoe kuwa, UNICEF kwa kushirikiana na Serikali, imefanya utambuzi wa shule ambazo zimeunganishwa na mtandao na itaendelea kufanya kazi na Serikali kwa lengo la kuhakikisha shule zote zinaunganishwa na mtandao ili wanafunzi wa kitanzania wananufaike na mtandao kitaaluma.
Akizungumza ofisini kwake na Bi. Wisch, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu - TAMISEMI Prof. Riziki Shemdoe ameahidi kuwa, ofisi yake itaendelea kushirikiana na UNICEF ili kuwezesha kukamilika kwa mpango wa kuanzisha na kuboresha shule mtandano nchini ambazo zitaleta tija kwa wanafunzi katika ujifunzaji na kwa walimu katika ufundishaji.
Katika kutimiza azma ya kuboresha shule mtandao, Prof. Shemdoe ameahidi kuendeleza ushirikiano na wadau wa sekta ya elimu ili kuhakikisha madarasa ya kidigitali yanaongezeka, na kwamba atakuwa mgeni rasmi kwenye uzinduzi wa mifumo ya kidigitali pindi itakapokuwa tayari kwa matumizi ya walimu na wanafunzi.
Aidha, Prof. Shemdoe ameahidi kuwa TAMISEMI itaendelea kushirikiana na Wizara ya Afya katika utekelezaji wa mpango wa Bima ya Afya kwa Wote (Universal Health Insurance), na kuongeza kuwa ofisi yake itahakikisha mifumo ya taarifa inasomana katika vituo vya afya na hospitali za wilaya.
Kikao kazi hicho cha Prof. Shemdoe na Bi. Elke Wisch, kimejadili maboresho katika sekta ya elimu, lishe, afya, ulinzi na usalama wa watoto, maji na usafi wa mazingira.




Comments
Post a Comment