TANZANIA, URUSI ZAJADILI MIKATABA YA KUBADILISHANA WAHALIFU NA KUHAMISHA WAFUNGWA


Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Huduma za Kisheria kwa Umma wa Wizara ya Katiba na Sheria, Ndugu Abdulrahaman Mshamu, ameongoza kikao cha kupitia mikataba mitatu ya ushirikiano kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Shirikisho la Urusi yenye lengo la kuimarisha ushirikiano wa kisheria na mapambano dhidi ya uhalifu wa kimataifa.

Mikataba hiyo imejumuisha Mkataba wa Kubadilishana Wahalifu (Extradition Treaty), Mkataba wa Kuhamisha Wafungwa Waliotiwa Hatiani (Transfer of Sentenced Persons) pamoja na Mkataba wa Ushirikiano katika Kulinda Raia dhidi ya Matumizi Mabaya ya Haki ya Kimataifa.


Kikao hicho kimewakutanisha wadau mbalimbali kutoka taasisi za Serikali ikiwemo Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Jeshi la Polisi Tanzania pamoja na Jeshi la Magereza Tanzania.

Upande wa Shirikisho la Urusi uliwakilishwa na Naibu Mkurugenzi wa Wizara ya Masuala ya Haki ya Urusi, Ndugu Evgeny Bulatov.

Akizungumza katika kikao hicho, Mshamu amesema mikataba hiyo inalenga kuimarisha ushirikiano wa kimataifa katika masuala ya sheria, usalama na haki, sambamba na kuwezesha wahalifu wanaotafutwa kurejeshwa katika nchi husika kwa ajili ya kuchukuliwa hatua za kisheria.

Aidha, amesema Mkataba wa Kuhamisha Wafungwa utasaidia wafungwa waliotiwa hatiani kutumikia vifungo vyao katika nchi zao, hatua inayochangia kulinda haki za wafungwa na kurahisisha ustawi wao wa kijamii na kifamilia.

Kwa upande mwingine, mikataba hiyo inatarajiwa kusaidia kuzuia wahalifu wa kimataifa kujificha katika nchi nyingine, kuimarisha mapambano dhidi ya uhalifu wa kuvuka mipaka pamoja na kuendeleza utawala wa sheria na ushirikiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na Urusi.

Kikao hicho ni sehemu ya jitihada za Serikali ya Tanzania kuendelea kuimarisha ushirikiano wa kimataifa katika sekta ya Sheria na Haki kwa manufaa ya wananchi na usalama wa mataifa yote
mawili.


Comments

Popular posts from this blog

RESIDENTS OF IYAGABUYAGA-BUSEGA URGED TO RESPECT WILDLIFE CONSERVATION LAWS

TANZANIA YAKAMILISHA MFUMO WA KUREJESHA HALI BAADA YA MAAFA

RC CHALAMILA MASHINDANO YA AFCON YATUMIKE KIBIASHARA