TANZANIA NA KENYA KUHARAKISHA UTEKELEZAJI MIRADI YA KUUNGANISHA NJIA ZA UMEME

Tanzania na Kenya zimekubaliana kuharakisha utekelezaji wa miradi mbalimbali ya njia za umeme zinazounganisha gridi za nchi hizo mbili pamoja na kuboresha mifumo ya usafirishaji wa umeme ili kuimarisha usalama wa nishati, kuongeza uhakika wa upatikanaji wa umeme na kukuza biashara ya umeme katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Makubaliano hayo yamefikiwa baada ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati anayeshughulikia Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Felchesmi Mramba, kufanya mazungumzo na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Mafuta wa Kenya, Bw. Alex Wachira, jijini Nairobi, Kenya.

Mazungumzo hayo yalijikita katika kuimarisha ushirikiano katika sekta ndogo ya umeme na nishati jadidifu, hususan biashara ya umeme, utekelezaji wa miradi ya uunganishaji wa gridi za umeme pamoja na maboresho ya mifumo ya usafirishaji na usambazaji wa umeme kati ya Tanzania na Kenya.

 Viongozi hao pia walijadili hatua mbalimbali za kuimarisha biashara ya umeme katika ukanda wa Afrika Mashariki kupitia Umoja wa Soko la pamoja la Kuuziana Umeme na Kuimarisha Mifumo ya Gridi-Eastern Africa Power Pool (EAPP).

Sambamba na hilo, Makatibu Wakuu hao walisisitiza umuhimu wa kuongeza wigo wa njia za usafirishaji umeme zitakazounganisha nchi hizo mbili kupitia maeneo ya Namanga, Lungalunga, Loitoktok na Isibania/Sirari.

Aidha, kikao hicho kilijadili pendekezo la kuanzishwa kwa mfumo wa Ring Circuit utakaojumuisha njia za Ibadakuli – Masaka, Ibadakuli – Kilgoris na Kilgoris – Masaka kwa lengo la kuongeza uthabiti wa gridi za umeme na kuimarisha biashara ya umeme kati ya Tanzania na Kenya.

Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Mafuta wa Kenya, Bw. Alex Wachira alieleza kuwa nchi hiyo imejipanga pia katika uwekezaji wa miundombinu ya gesi asilia kwa lengo la kuimarisha upatikanaji wa nishati hiyo nchini humo, pia kuongeza ushirikiano wa kikanda katika sekta ya nishati.

Comments

Popular posts from this blog

RESIDENTS OF IYAGABUYAGA-BUSEGA URGED TO RESPECT WILDLIFE CONSERVATION LAWS

MATIVILA URGES CONTRACTOR TO DELIVER MOHORO BRIDGE ON SCHEDULE