RAIS SAMIA AWASILI RWANDA KUSHIRIKI MKUTANO WA NISHATI YA NYUKLIA
Mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kigali, Mkuu wa Nchi akipokelewa na viongozi mbalimbali wa kiserikali akiwemo Waziri wa Nishati wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi, ambaye ameambatana na jopo la wataalamu wa sekta hiyo kutoka nchini.
Mkutano huo wa kimkakati wa NEISA 2026 unafanyika nchini Rwanda kuanzia Mei 18 hadi Mei 21, 2026, ukikutanisha Wakuu wa Nchi, Mawaziri wa Nishati, wanasayansi, na wadau wakubwa wa kimataifa wa masuala ya teknolojia na nishati.
Lengo kuu la mkutano huo ni kujadili uvumbuzi, fursa, na changamoto za matumizi salama ya nishati ya nyuklia kama chanzo mbadala na cha uhakika cha nishati ili kuchochea mapinduzi ya viwanda na maendeleo ya kiuchumi barani Afrika.
Ushiriki wa Rais Samia unakuja wakati ambapo Tanzania ipo mstari wa mbele katika kutafuta na kuwekeza kwenye vyanzo mbalimbali vya nishati ili kukidhi mahitaji yanayokua kwa kasi ya soko la ndani na kikanda. Kupitia mkutano huu, Tanzania inatarajiwa kubadilishana uzoefu na mataifa mengine kuhusu namna ya kuingiza nishati ya nyuklia kwenye gridi za taifa kwa njia salama na endelevu.
Chini ya uongozi wa Rais Samia, Tanzania imeendelea kuonekana kama kinara katika diplomasia ya kiuchumi na nishati barani Afrika. Uwepo wa Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi, unathibitisha dhamira ya wizara hiyo katika kufuatilia kwa karibu teknolojia mpya zinazoweza kupunguza gharama za uzalishaji wa umeme na kulinda mazingira.
Mkutano huu unatarajiwa pia kutoa fursa kwa Tanzania kujenga ushirikiano na mashirika ya kimataifa yanayosimamia nishati ya nyuklia duniani (IAEA) kwa ajili ya mafunzo na ujenzi wa uwezo wa wataalamu wa ndani wa masuala ya sayansi ya nyuklia.



Comments
Post a Comment