NEMC YAIMARISHA USHIRIKIANO NA BENKI YA DUNIA KATIKA MIRADI YA KIMKAKATI YA MAZINGIRA

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limekutana na ujumbe wa Benki ya Dunia ulioongozwa na Mkurugenzi wa Kanda ya Afrika Mashariki na Kusini, Bi Anna Wellenstein pamoja na Bw. Muhammad Kandeel, kwa lengo la kujadili namna ya kuimarisha ushirikiano katika kuboresha mifumo ya usimamizi wa mazingira nchini.

Majadiliano hayo yalijikita katika maeneo mbalimbali ikiwemo kuimarisha utekelezaji wa tathmini za athari kwa mazingira, kujenga uwezo wa wataalamu wa mazingira na maafisa wa serikali, pamoja na kuwawezesha wadau mbalimbali kuelewa na kutumia kwa ufanisi mifumo na taratibu za Benki ya Dunia katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo. Timu ya NEMC iliongozwa na Mkurugenzi Mkuu, Dkt. Immaculata Semesi.

Katika kikao hicho, NEMC ilitoa shukrani kwa Benki ya Dunia kwa ushirikiano wake mkubwa katika utekelezaji wa Mradi wa Kudhibiti Matumizi ya Zebaki kwa Wachimbaji Wadogo (EHPMP), ambao umeleta mafanikio makubwa katika kuimarisha usimamizi wa kemikali na kupunguza athari za zebaki katika shughuli za uchimbaji mdogo wa dhahabu nchini.

Kwa upande wake, Benki ya Dunia ilieleza kuridhishwa na matokeo ya mradi huo na kuahidi kuendelea kutoa ushirikiano wa karibu katika kufuatilia na kuendeleza mafanikio yaliyopatikana kupitia mradi huo.



Comments